Monday, 2 September 2013

MWANAMUZIKI AFUNGWA MIEZI 21 KWA KUWATUKANA POLISI

MWANAMUZIKI ALA YAACOUBI

Mwanamuziki wa kizazi kipya nchini Tunisia amehukumiwa kifungo cha miezi 21 jela kwa kuwatusi polisi , miezi miwili tu baada ya kuachiliwa kufuatia maandamano ya umma.
Ala Yaacoubi, anayesifika kwa jina Weld El 15, alifungwa jela miaka miwili mnamo mwezi Juni kwa kutoa wimbo uliokuwa unawafananisha polisi na Mbwa ambao unasema kuwa polisi wanapaswa kunyongwa.
Hata hivyo hukumu yake iliondolewa mwezi Julai alipoachiliwa ingawa inadaiwa kuwa aliendelea kuimba wimbo huo.
Hukumu hii imetolewa wakati yeye mwenyewe hakuwa mahakamani na kwa hivyo atahitajika kujikabidhi kwa polisi.
Wakili wake anasema kuwa kesi hiyo ilihusu zaidi kushambulia uhuru wa watu kujieleza.
"nitazungumza na mteja wangu kupinga uamuzi huu , lakini hukumu zinazotolewa dhidi ya wasanii zinaonyesha kuwa vita dhidi ya ukandamizaji wa uhuru wa wasanii kujieleza vitaendelea,'' alisema wakili huyo Ghazi Mrabet.
Alisema kuwa yeye pamoja na mteja wake hawakufahamishwa chochote kuhusu kesi hii.
Msanii mwingine Klay BBJ, alihukumiwa pamoja na Weld El 15.
Ingawa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 25, hakujulikana sana , kesi yake bila shaka imempa umaarufu baada ya wakereketwa wa haki za binadamu kumwakilisha huku waandishi na wanablogu wakiizungumzia sana.
Wananchi wa Tunisia walichagua serikali ambayo ina msimamo wa kadri baada ya kuondolewa mamlakani kwa rais aliyeitawala nchi hiyo tangu mwaka 2011 Zine al-Abidine Ben Ali.

No comments:

Post a Comment