Katika
kipindi cha miaka mitano tu iliyopita, serikali imetumia zaidi ya Sh.
23 bilioni kujitetea, kwa kulipa makampuni ya uwakili. Gharama hizi
zinaongezeka mwaka hadi mwaka kufuatia kesi kuchukua muda mrefu na hata
kufumuka kwa kesi mpya.
Sehemu ya mabilioni hayo ya shilingi imelipwa kwa makampuni ya
wanasheria ya Mkono and Company Advocates ya Tanzania na Hunton and
William ya Marekani kwa kutetea TANESCO iliyoshitakiwa na kampuni ya
Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Mabilioni mengine yamelipwa kwa makampuni ya mawakili ya Rex Attorney ya
Tanzania na Reed Smith ya Uingereza kwa kutetea TANESCO katika kesi
iliyofunguliwa na kampuni ya Richmond Development Company (LLC).
Rex Attorneys na Reed Smith wamelipwa au watalipwa pia mabilioni ya
shilingi kwa kutetea TANESCO katika shauri lililofunguliwa na makampuni
ya Dowans Holdings S.A na Dowans Tanzania Limited (DTL) katika mahakama
ya kimataifa ya usuluhishi wa kibiasha (ICC).
Nyaraka zinaonyesha kuwa tayari Mkono and Company Advocates na Hunton
and William wamelipwa na TANESCO kiasi cha dola 11,818,542.89 (sawa na
karibu Sh. 17 bilioni).
Kampuni ya Mkono and Company Advocates inamilikiwa na mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono.
Aidha, kampuni ya Mkono imelipwa pia kiasi cha Sh. 8.5 milioni kwa
kusimamia shauri lililofunguliwa na benki ya Standard Chartered Bank ya
Hong Kong dhidi ya serikali katika shauri la kukatisha mkataba wa IPTL.
Serikali na IPTL waliingia mkataba mwaka 1994.
Nyaraka zinaonyesha kuwa Rex Attoney na mwenzake walilipwa kiasi cha
dola 3,574,351.51 (karibu Sh. 5 .2 bilioni) katika shauri
lililofunguliwa na makampuni ya Dowans Holdings S.A na Dowans Tanzania
Limited (DTL) katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa kibiasha
(ICC).
Mawakili hao pia wamelipwa dola 860,056.71 (karibu sawa na shilingi 1.2
bilioni) kwa kazi ya kutetea TANESCO dhidi ya kesi iliyofunguliwa na
kampuni ya Richmond Development Company (LLC) na kusikilizwa katika
Falme za Kiarabu.
Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja mwezi mmoja baada ya mbunge wa Bumbuli
(CCM), January Makamba kuibua kile kilichoitwa, “taarifa juu ya
upatikanaji wa umeme nchini,” ambapo tarehe 3 Februari 2011 alitaka
waziri wa nishati na madini, William Ngeleja kueleza hatua
zinazochukuliwa na TANESCO katika kukabiliana na mgawo wa umeme na mzigo
wa kesi unaolikabili.
Katika barua hiyo, Makamba anasema, “Katika viambatanisho vya hukumu ya
ICC, kama ilivyosajiliwa mahakama kuu ya Tanzania zipo nyaraka
zinazoonyesha kwamba mwanasheria aliyeishauri TANESCO kuvunja mkataba na
Dowans – kwa kusema kwamba siyo mkataba halali na kwamba hakuna madhara
ya kisheria kuuvunja – ndiye huyohuyo pia aliyeshauri benki ya Stanbink
kutoa mkopo wa dola za 120 kwa Dowans – kwa kusema kwamba ni kampuni
halali, inakopesheka na ina mkataba halali na TANESCO.”
Anasema, “Ni mwanasheria huyohuyo aliyewakilisha TANESCO kwenye kesi
iliyofunguliwa na Dowans, kesi ambayo ilitokana na ushauri wake, na
baada ya hukumu ndiye huohuyo, kwa mujibu wa maelezo yako mheshimiwa
waziri ya tarehe 6 Januari 2011, aliyetoa ushauri kwamba hakuna njia
nyingine zaidi ya kuilipa Dowans.”
Makamba alitaka serikali kueleza suala hilo kwa ufasaha ili kuondoa kile
alichoita, “picha inayoweza kuonyesha serikali ilikosa umakini kwenye
jambo hili zima na maadili hayakuzingatiwa.”
Alisema itakuwa vema taarifa ya serikali ikieleza ni wanasheria gani
waliotumiwa na TANESCO kwa kila hatua katika shauri lake Dowans kwa
kuanzia kwenye ushauri na kabla ya kuvunjwa kwa mkataba.
Akijibu hoja za Makamba, Ngeleja anakiri kuwa benki ya Standard
Chartered ya (Hong Kong) ambayo ni benki tanzu ya Standard Chartered ya
Uingereza inayomiliki asilimia kubwa ya hisa za IPTL Tanzania Ltd.,
wameishitaki serikali kwa madai ya kutumia mitambo yake ya kuzalisha
umeme kupitia Provisional Liquidator hivyo kukiuka Bilateral Investment
Treaty (BIT) kati yake na serikali ya Uingereza.
Kesi hizo ni Na. ARB /10/20 iliyofunguliwa na Standard Chartered Bank
(Hong Kong) dhidi ya TANESCO, tarehe 1 Oktoba 2010 na kesi Na.ARB/10/12
iliyofunguliwa tarehe 11 Juni 2010.
Katika shauri hilo, IPTL wanataka mahakama “iamuru serikali kutoa tamko
la kukiri kukiuka mkataba wa uwekezaji wa kimataifa – Bilateral
Investment Treaty (BIT) na kulipa fidia ya dola 118.6 milioni, pamoja na
kulipa gharama zote za uwekezaji - capacity charges – ambazo shirika
hilo hazijazilipa tokea mwaka 2007 pamoja na fidia ya dola 130 milioni.”
Ngeleja anasema chimbuko la kesi hizo ni mgogoro wa awali kati ya Taneso
na na IPTL ambao uliwasilishwa ICSID, Novemba mwaka 2007. Kesi
zilizotajwa ziko katika hatua za awali na zinatarajiwa kuanza
kusikilizwa Aprili mwaka huu.
Akijibu madai ya njia iliyotumika kupatikana kwa makampuni ya
wanasheria, Ngeleja anasema “TANESCO iliona ni busara kuendelea
kuwatumia mawakili walewale (Mkono and Company Advocates) kwa kuwa wana
taarifa muhimu kuhusiana na kesi husika.
Anasema, “Kampuni ya Mkono ilianza kushughulikia shauri la IPTL tangu
mwaka 2007 baada ya kupendekezwa na serikali kuwa washauri wa Kamati ya
serikali ya ununuzi wa deni la IPTL. Kutokana na uelewa wa mawakili hao
juu ya IPTL, ilionekana ni busara waendeshe kesi hiyo.”
Kuhusu kampuni ya wanasheria ya Rex Attorney, Ngeleje anasema, ilipewa
kazi ya ushauri baada ya ushindani uliohusisa kampuni tatu za FK Law
Chambers, IMMA Advocates na Mkono. Anasema katika shauri la Dowans,
TANESCO waliamua kuichukua tena Rex kwa ilikuwa na uzoefu na mkataba
huo.
Katika shauri hilo, mahakama ya ICC imeamuru TANESCO kulipa kiasi cha
dola 94 milioni (Sh. 134 bilioni) kutokana na kushindwa katika kesi
hiyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa MwanaHALISI, kampuni ya Mkono ililipwa na
TANESCO – miezi miwili kabla ya uchaguzi, 19 Agosti 2010 kiasi cha dola
1,088,550.00 (karibu Sh.1.6 bilioni). Malipo hayo yalifanywa kupitia
ankara Na. 124/10.
Aidha, kabla ya Mkono kuchukua kitita hicho cha fedha, tarehe 15 Julai
2009, TANESCO walilipa mwanasheria huyo kiasi cha dola 2,177,100.00
(karibu Sh. 3.7 bilioni). Fedha hizo zililipwa kupitia ankara Na. 069/09
kwa kile kilichoitwa kazi za usuluhishi kati ya TANESCO na IPTL.
Nayo Rex Attonery, imelipwa na TANESCO kiasi cha dola 47,552.25 kupitia
ankara Na. 456/10 ya 28 Septemba 2010 kwa kazi za ushauri katika kesi
Na. 15910 iliyofunguliwa na kampuni ya Richmond katika mahakama ya ICC
dhidi ya TANESCO. Malipo mengine ya dola 472,000.00 yamefanyika 23 Juni
2010 kupitia ankara Na. 34/10 kwa ajili ya masuala ya usuluhishi katika
kesi Na. 15910 kati ya TANESCO na Richmond. Dola 83,504.46 zililipwa
tarehe 9 Aprili 2010 kama gharama za kukodishia chumba cha kusikilizia
usulihushi kati ya TANESCO na Richmond kwa kesi hiyohiyo.KWA MSAADA WA JAMII FORUM
No comments:
Post a Comment